KISA MUKWALA,SOWAH…PANTEV AWASHIWA MOTO SIMBA…….

KISA MUKWALA,SOWAH…PANTEV AWASHIWA MOTO SIMBA…….

 

Habari za Simba leo

KOCHA wa Petro Atletico ameondoka na furaha baada ya kuichapa Simba, lakini kuna kitu amesema lazima kitakoleza moto mbaya wa mwenzie Dimitar Pantev aliyepo Msimbazi.

Petro iliifunga Simba kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa katika mechi yao ya ufunguzi ya Kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa ni mara ya kwanza kwa Wekundu hao kupoteza nyumbani tangu Februari 18, 2023 ilipolala 3-0 mbele ya Raja Casablanca ya Morocco.

Akizungumza  mara baada ya mechi hiyo ya juzi, kocha Francesc Artiga alisema kadiri ya muda ulivyokuwa unakwenda, waliona hakuna ulazima wa kuendelea kujilinda.

Artiga, raia wa Hispania, alisema waliifanyia tathmini ya kina Simba na kitendo cha wekundu hao kuanza mechi hiyo bila ya washambuliaji halisi iliwapa nafasi ya kubadilika na kuanza kutafuta mabao kwa tahadhari.

Simba iliwaacha nje ya kikosi cha kwanza washambuliaji watatu wa kati, Steven Mukwala, Jonathan Sowah na Seleman Mwalimu ‘Gomes’, uamuzi wa benchi la ufundi ambao umekosolewa sana.

“Ilikuwa nzuri kwetu kuona Simba wameanza bila washambuliaji halisi na tulikuwa na kazi kubwa ya kuwasoma kabla ya kuja Tanzania. Simba ni timu nzuri hasa inapokuwa nyumbani,” alisema Artiga na kuongeza;

“Tuliwasoma sana aina ya washambuliaji wao, lakini walikuwa wanacheza kwa tahadhari sana, baadaye tukaona inawezekana kujaribu kwenda kwao na tukafanya hivyo.”

Aidha, Artiga aliongeza ushindi huo ni kitu muhimu kwao lakini wamejifunza kwamba wanatakiwa kuwa makini zaidi kwa kuwa licha ya kuwafunga Simba lakini wamekutana na viungo bora.

“Ndio tumeshinda hii mechi lakini tumejifunza kitu kwamba tunatakiwa kuwa makini na timu yenye viungo wazuri kama wale wa Simba, wana kasi sana kama hautakuwa makini na wanaweza kukupa tatizo.“Tulilazimika kuwa makini na hesabu zao lakini hata baadaye walipoanza kuwapa nafasi washambuliaji wao tulihakikisha hawapati nafasi ya kufanya uamuzi sahihi jirani na eneo la hatari,” alisema Artiga anayeenda kuisubiri Esperance ya Tunisia katika mechi ijayo ikiwa nyumbani.

Simba kwa upande wao itasafiri hadi Bamako, Mali kukabiliana na wenyeji wao Stade Malien mechi zote zikipigwa Ijumaa.

Post a Comment

0 Comments