UZINDUZI WA YANGA SOCCER SCHOOL WAFANA DAR, MOSIMANE ASEMA NI WAZO LAKE KWA HERSI

UZINDUZI WA YANGA SOCCER SCHOOL WAFANA DAR, MOSIMANE ASEMA NI WAZO LAKE KWA HERSI

 

KOCHA wa Kimataifa wa Afrika, Pitso John Hamilton Mosimane amesema kwamba uanzishwaji wa shule ya soka ya Yanga ni wazo lake ambao alimshauri Rais wa klabu hiyo, Hersi Ally Said Agosti mwaka 2022.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo wakati wa uzinduzi wa shule hiyo ambayo itajulikana kama Yanga Soccer School ulofanyika Uwanja wa Speed Sports, Muhimbili Centre – Mosimane mshindi wa mataji ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na klabu za mamelodi Sundowns ya kwao na Al Ahly ya Misri amesema alitoa ushauri huo alipokuja nchini kwenye kilele cha tamasha la Wiki ya Mwananchi Agosti 6, mwaka 2022.
“Siku ya mwananchi Day nilivutiwa sana na mwamko wa mashabiki. Tukiwa kwenye gari nikamwambia Rais wa Yanga anzisha Shule ya Soka. Nimefurahi sana hatimaye leo nipo kwenye uzinduzi,” amesema Mosimane ambaye pia ni kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’.
Aidha, Kocha huyo wa zamani wa Al Ahli Jeddah ya Saudi Arabia, Abha za Saudi Arabia, Al Wahda ya Abu Dhabu, Falme za Kiarabu (UAE) na Esteghlal ya Iran amempongeza Mtendaji Mkuu wa Yanga SC, Andre Mtine raia wa Zambia.

“Pongezi za kipekee kwa rafiki yangu wa muda mrefu sana, Andre Mtine. Mtine ana uzoefu mkubwa wa soka la Afrika. Amefanya kazi kubwa iliyotukuka huko DR Congo akiwa na Mazembe. Nadhani kila mtu anatambua mafanikio ya Mazembe huwezi kusahau mchango wake. Hongera sana kwa kazi kubwa unayowafanyia wana Yanga,”amesema na kuongeza;
“Namshukuru sana Rais wa Yanga SC, Mimi na Injinia ni marafiki wa muda mrefu sana. Niliwahi kuja hapa kwa ajili ya Mwananchi Day. Ama kwa hakika ni siku pekee na ya kufana sana. Mashabiki wa Yanga wanaipenda sana timu yao. Hongereni sana. Nyie ni mfano wa kuigwa,”.

Awali, Raia wa Yanga SC, Hersi Said alisema kwamba Yanga Soccer School ni jukwaa litakalowaleta watu wataaluma tofauti tofauti, vijana wanaotengenezwa hapa wataondoka wakiwa na maarifa ya kutosha.
“Tunatengeneza vijana wa kesho ambao wanapenda mpira lakini wanaujua vyema na jamii ya kesho itakwenda kuupenda mpira na kuushabikia. Niwapongeze sana wazazi ambao wametuamini na kuleta vijana wao kuwasijili kwenye 𝐘𝐚𝐧𝐠𝐚 𝐒𝐨𝐜𝐜𝐞𝐫 𝐒𝐜𝐡𝐨𝐨𝐥. Jukwaa hili ni jukwaa muhimu sana kwa ukuaji wa soka la kizazi cha kesho,”amesema Hersi.
Hersi amesema watoto hao watakuwa msaada mkubwa kwa familia zao na kwa taifa kwa ujumla kupitia soka yao baadaye, kwani mradi huo wa 𝐘𝐚𝐧𝐠𝐚 𝐒𝐨𝐜𝐜𝐞𝐫 𝐒𝐜𝐡𝐨𝐨𝐥 ni endelevu ambao unachukua watoto wa kuanzia umri wa miaka chini ya miaka 11, U-13 na U-15.

“Hatutaishia mkoa wa Dar Es Salaam pekee yake bali tutatanua wigo kwa maeneo mbalimbali Tanzania. Jukwaa hili litatusaidia sana kwenye kuinua vipaji ambavyo tunaweza kuvitumia kwenye timu zetu za vijana. “Tumeongea na Kocha Pitso Mosimane ambaye amekubali ombi letu la kutoa mafunzo kwa makocha wetu wa vijana,”.
“ Lengo letu ni kutumia falsafa ya timu yake ya soka na kuimarisha falsafa yetu pia hapa. Tunamshukuru sana Kocha Mosimane kwa kukubali wito wa kujiunga nasi siku hii ya historia,” amesema.

Uzinduzi huo ulifana ukihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wachezaji wa vikosi vya Yanga kwa wanaume na wanawake pamoja na wa timu za vijana na makocha wao.

Post a Comment

0 Comments