Mastaa wa muziki na taaluma zao za elimu kabatini

Mastaa wa muziki na taaluma zao za elimu kabatini

 Mastaa wa muziki na taaluma zao za elimu kabatini


Kwa muda mrefu kumekuwa na dhana kwamba wasanii wengi wa muziki hawana elimu ya juu, na kwamba vipaji ndio vinawabeba na kuwakutanisha na watu wakubwa lakini watu hao hao wanasahau kuwa taaluma walizosomea ndio huwabeba mara zote.

Wengi wao walisoma vyuo vikuu ndani na nje ya nchi, wakijipatia ujuzi katika taaluma tofauti ambazo zimewasaidia katika safari yao ya muziki. Na hapa nakusogezea orodha ya baadhi ya wasanii na kozi ambazo walisomea huku wengine wakifanya kazi kwa muda kupitia taaluma hizo kabla ya kugeukia kwenye muziki.

Burna Boy
Nyota huyo ambaye kwasasa anatajwa kuwa miongoni mwa wakali wa muziki wa Afrika alisomea ‘Media Technology’ katika Chuo Kikuu cha Sussex na baadaye akabadilisha kozi na kusomea ‘Media Communications & Culture’ katika chuo kikuu cha ‘Oxford Brookes’, vyuo vyote vinavyopatikana nchini Uingereza. Hata hivyo kabla ya kurudi Nigeria na kujikita katika muziki aliwahi kufanya kazi katika redio ya Rhythm 93.7 FM huko Port Harcourt.

Davido
Mkali huyo wa Afrobeat ambaye amepata uteuzi kwenye kinyang’anyiro cha tuzo kubwa zaidi duniani Grammy katika kipengele cha ‘Best African Music Performance’ alihitimu ‘Bachelor of Arts in Music’ katika Chuo Kikuu cha Babcock, kilichopo Nigeria, mwaka 2015. Ingawa alisomea muziki rasmi hakuwahi kufanya kazi nje ya jukwaa kutokana na muziki kuwa ndio taaluma yake kuu.

Tangu kuanza kwake muziki amewahi kutamba na ngoma mbalimbal ikiwamo Unavailable, Fall, Blow My Mind, FIA huku album yake ya Timeless ikiendelea kupata streaming nyingi katika mitandao ya kusikiliza muziki.

Wizkid
Alianza safari yake ya elimu katika chuo cha Lagos State University (LASU) na baadaye alihamia Lead City University akichukua kozi ya ‘International Relations’, hata hivyo hakuchukua muda mrefu aliacha chuo ili kufuata ndoto zake za kuwa mwanamuziki mkubwa ambapo awali familia na watu wa karibu hawakukubaliana na hilo.

Lakini kupitia bidii na ubunifu wake katika muziki, Wizkid amekuwa mmoja wa wasanii wakubwa zaidi barani Afrika, akipenya kwenye majukwaa ya kimataifa kama Billboard Hot 100 na kushirikiana na mastaa wakubwa kama Drake, Beyoncé, na Justin Bieber.

Tiwa Savage
Mwanamuziki huyo ambaye anajulikana kama Queen of Afrobeats, alianza kusomea Business Administration katika University of Kent nchini Uingereza na baada ya kuhitimu masomo yake aliamua kufuata ndoto zake za kuwa msanii mkubwa ambapo alikwenda kusomea kozi ya Music katika Berklee College of Music nchini Marekani na kabla hajaanza kujikita katika muziki alishawahi kufanya kazi katika benki ya ‘Royal Bank of Scotland’ kama mhasibu.

Asake
Mkali huyo ambaye anatambulika zaidi kwa kubadilisha mwonekano kila baada ya miezi kadhaa ni muhitimu katika chuo cha ‘Obafemi Awolowo University’ akichukua kozi ya ‘Theatre and Performing Arts’. Kwa kuwa elimu yake inaendana kabisa na kipaji chake inaelezwa kuwa elimu hiyo imemsaidia katika kuboresha show zake hasa kwenye ziara pamoja na maonesho mbalimbali.

Ayra Starr
Staa huyo anayeng’aa chini ya lebo ya Mavin Records, alisoma International Relations and Political Science katika chuo cha Les Cours Sonou nchini Benin akiwa na umri wa miaka 14 pekee. Ingawa hakuwahi kufanya kazi kwenye taaluma hiyo, elimu hiyo imempa upeo mpana wa dunia unaoonekana kwenye mashairi yake.

Kizz Daniel
Msanii huyo ambaye amewahi kutamba na ngoma kama Buga, Yeba, One Ticket na nyinginezo anatajwa kuwa na shahada ya ‘Water Resources Management and Agrometeorology’ aliyoipata katika chuo cha ‘Federal University of Agriculture’ huko Abeokuta. Na baadaye aliamua kuchagua muziki huku akiripotiwa kutowahi kujihusisha wala kufanya kazi katika taaluma hiyo.

Post a Comment

0 Comments