KAPOMBE NJE TUZO YA MWANASOKA BORA ANAYECHEZA AFRIKA

KAPOMBE NJE TUZO YA MWANASOKA BORA ANAYECHEZA AFRIKA

 

BEKI wa Simba SC, Shomari Salum Kapombe ametupwa nje ya kinyang’anyiro cha Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka Anayecheza Klabu ya Afrika.
Katika Tuzo hizo za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) — Kapombe amezidiwa kete beki mwenzake wa kulia, Mmorocco Mohamed Chibi na washambuliaji, Mkongo Fiston Mayele, wote wa Pyramids ya Misri na Oussama Lamlioui wa RS Berkane ya kwao, Morocco.
Wengine sita walioteuliwa awali kuwania Tuzo ni Ismael Belkacemi (Algeria/Al Ahli Tripoli), Blati Toure (Burkina Faso/Pyramids FC), Issoufou Dayo (Burkina Faso/RS Berkane), Ahmed Samy (Egypt/Pyramids), Emam Ashour (Egypt/Al Ahly), Ibrahim Adel (Egypt/Pyramids) na Mohamed Hrimat (Morocco/AS FAR).
Ikumbukwe Simba SC nayo imetupwa nje ya kinyang’anyiro cha Tuzo ya Klabu Bora ya Mwaka ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) — ikizidiwa kete na Pyramids ya Misri, RS Berkane ya Morocco na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini zilizoingia Fainali.
Simba ni kati ya timu 10 zilizoteuliwa awali kuwania Tuzo hiyo — nyingine sita ni CR Belouizdad, CS Constantine zote za Algeria, ASEC Mimosas ya Ivory Coast, Orlando Pirates, Stellenbosch za Afrika Kusini na Al Hilal ya Sudan.
Aidha, mshambuliaji wa Yanga Clement Francis Mzize pia ameingia kwenye orodha ya awali ya Tuzo ya Bao Bora Afrika kutokana na bao lake katika ushindi wa 3-1 dhidi ya TP Mazembe Januari 4 mwaka jana kwenye mchezo wa Kundi A Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Siku hiyo Mzize alifunga mabao mawili na linalowania Tuzo hiyo ni la kwanza alilofunga dakika ya 33 ambalo lilikuwa la kusawazisha kufuatia kipa Msenegal, Aliouane Badara Faty kuanza kuifungia TP Mazembe kwa mkwaju wa penalti dakika ya 16.
Mzize aliifungia Yanga bao la tatu pia dakika ya 60 baada ya kiungo mshambuliaji wa Kimataifa wa Burkina Faso, Stephane Aziz Ki ambaye kwa sasa amehamia Wydad Athletic ya Morocco kuifungia Yanga bao la tatu dakika ya 56.

Post a Comment

0 Comments