Ja Rule: uhasama na 50 Cent uliharibu Hip Hop

Ja Rule: uhasama na 50 Cent uliharibu Hip Hop

 Ja Rule: uhasama na 50 Cent uliharibu Hip Hop

Msanii wa Hip Hop Marekani, Ja Rule (49), amefunguka kuhusu uhasama (beef) wa muda mrefu kati yake na rapa mwenzake, 50 Cent, 50 akisema kuwa vita vyao vya maneno viliwagawa wasanii wa New York.

Ja Rule, mkali wa kibao cha Always On Time (2001), amesema vita hivyo vilivyotikisa tasnia ya muziki mwishoni mwa miaka ya 1990 na mwanzoni mwa 2000, viliathiri vibaya muziki wa jiji hilo.

Akizungumza na Podcast ya 7PM in Brooklyn iliyoongozwa na Carmelo Anthony, Ja Rule alisema kuwa chuki iliyokuwepo kati yake na 50 Cent ilivunja umoja uliokuwa unaiunganisha tasnia ya rap ndani ya New York.

"Ugomvi wangu na 50 Cent ulivuruga sana Hip Hop ya New York. Kwa kweli, ulifanya hivyo kwa sababu uliwagawa wasanii wengi wa New York wakati huo," alisema Ja Rule kutokea mitaa ya Queens.

Rapa huyo alifananisha uhasama wao na ule wa sasa kati ya Kendrick Lamar na Drake, akisema kuwa migogoro ya namna hiyo haiwezi kuleta faida yoyote katika tasnia ya muziki.

"Angalia kama ilivyo kwa Kendrick na Drake. Hakuna kitu kizuri kinachotokana na mambo haya," alisema Ja Rule, ambaye aliwahi kumchana 50 Cent kupitia nyimbo kama Life's on the Line na Back Down.

Hata hivyo, Ja Rule alikiri kuwa licha ya athari hizo za uhasama wao, bado anaamini alikuwa msanii bora zaidi kwa wakati huo kuliko mshindani wake.

"Niliamini mimi ndiye nilikuwa rapa bora. Nilitengeneza nyimbo bora zaidi, na nahisi nyimbo zangu bado zinaishi hadi muda huu zikifanya vizuri," alisema Ja Rule kwa kujiamini.

Pamoja na hayo, Ja Rule alimpa mpinzani wake heshima anayostahili akisema mwisho wa siku, lazima uwaheshimu watu wote hata kama huwapendi wote, lazima uone thamani kwa wote.

Uhasama kati ya Ja Rule na 50 Cent uliwahi kuwa miongoni mwa migogoro mikubwa zaidi katika historia ya Hip Hop, ukiandamana na nyimbo za matusi na malumbano ya hadharani.
Chanzo cha uhasama wao kinahusisha mchanganyiko wa migogoro ya mitaani, wivu wa mafanikio, na masuala ya biashara ya muziki.

Wakati huo, Ja Rule alikuwa akitamba kupitia lebo ya Murder Inc., 50 Cent, ambaye bado alikuwa anajaribu kutoka kimuziki, alihisi Ja Rule na kundi lake walikuwa wanamdharau na kumzuia kupata nafasi kwenye Hip Hop ya New York.

Ila kadiri 50 Cent alivyozidi kupata umaarufu kupitia albamu yake, Get Rich or Die Tryin' (2003), ndivyo na uhasama wao ulizidi kuongezeka. Wakati huo huo, lebo ya Murder Inc. ilianza kuyumba kutokana na matatizo ya kisheria huku 50 Cent akiendelea kuwashambulia na kundi lake la G-Unit.

Post a Comment

0 Comments