YANGA SC YAANZISHA SHULE YA SOKA ADA YA KUJIUNGA SH 600,000, KILA MWEZI 400,000

YANGA SC YAANZISHA SHULE YA SOKA ADA YA KUJIUNGA SH 600,000, KILA MWEZI 400,000

 

KLABU ya Yanga imeanzisha mradi wa soka ya vijana, 𝐘𝐚𝐧𝐠𝐚 𝐒𝐨𝐜𝐜𝐞𝐫 𝐒𝐜𝐡𝐨𝐨𝐥 ambayo itazinduliwa rasmi Novemba 15, mwaka huu.
Akizungumza kwenye Mkutano na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa klabu ya Yanga, Andrew Mtine amesema kwamba mradi huu unakwenda kugusa ukuaji wa soka la vijana hapa nchini.
“Tuna watoto wengi sana ambao wana ndoto za kuwa wachezaji lakini wanakosa daraja sahihi. Shule hii ya soka itajumuisha watoto wa umri wa U-11, U-13 na U-15. Mfumo huu wa 𝐘𝐚𝐧𝐠𝐚 𝐒𝐨𝐜𝐜𝐞𝐫 𝐒𝐜𝐡𝐨𝐨𝐥 ni moja kati ya nyenzo imara ambazo zinatumika na vilabu vikubwa duniani,”.
Mtine amesema kutokana na umuhimu wa mradi huo, wamekaribisha wadau mbalimbali siku ya uzinduzi, akiwemo Pitso Mosimame, Kocha wa zamani Mamelodi Sundowns ya kwao, Afrika Kusini na Al Ahly ya Misri.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Michezo wa Yanga SC, Paul Mathew amesema kwamba 𝐘𝐚𝐧𝐠𝐚 𝐒𝐨𝐜𝐜𝐞𝐫 𝐒𝐜𝐡𝐨𝐨𝐥 ni daraja la kipekee la kutimiza ndoto za watoto wanaotamani kuwa wanasoka.
“Kupitia mradi huu tunaweza kupata vijana ambao baadhi yao wanaweza kujiunga na timu zetu za U-17 na U-20. 𝐘𝐚𝐧𝐠𝐚 𝐒𝐨𝐜𝐜𝐞𝐫 𝐒𝐜𝐡𝐨𝐨𝐥 ni sehemu ambayo mtoto atapata maarifa sahihi ya soka. Tunakwenda kuanzisha mtaala maalum wa kumnoa mtoto. Yanga ni taasisi inayoheshimika. Hivyo ukimleta mtoto wako hapa utakuwa umemjengea mazingira sahihi kiusalama na kitaalum”, amesema Paul Mathew na kuongeza;
“Huu ni ubunifu mkubwa sana ambao utatoa fursa kwa vijana wadogo kuonesha vipaji vyao na kupata elimu sahihi ya soka. Tunakwenda kuanzisha msingi imara kutoka kwa wataalam wakubwa ili kumuandaa mtoto kufikia ndoto zake. Tuna matumaini kuwa kupitia mradi tunakwenda kuzalisha magwiji mbalimbali wa soka”.

Naye Mkurugenzi wa Mashindano wa klabu ya Yanga, Ibrahim Mohamed Said amesema Ada ya kujiunga na Yanga Soccer School itakuwa Sh. 600,000 kwa mwezi wa kwanza, kiasi cha Sh. 50,000 kikitumika kama ada ya usajili, 150,000 kwa ajili ya vifaa na 400,000 kama ada ya mafunzo.
“Ukishalipa ada ya 600,000 mwezi wa kwanza, mwezi unaofuata utalipa kiasi cha Tsh 400,000. Fomu zinapatikana hapa Jangwani. Kwa mawasiliano zaidi unaweza kuwasiliana kupitia namba +𝟐𝟓𝟓 𝟔𝟕𝟑 𝟎𝟔𝟖 𝟖𝟑𝟗,” amesema.


Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu ya Yanga, Ally Kamwe amesema kwamba wameamua kuanzisha soccer school kwa sababu kuna watoto wengi wana uhitaji mkubwa.
“Sensa inaonyesha kuwa watoto kuanzia 0-13 wapo milioni 20. Katika kundi hili tunafahamu wapo baadhi yao ambao wanatamani kucheza mpira. Wazazi wengi wamekuwa wakijaribu kutafuta maeneo ambayo watoto wao wangepata mafunzo ya soka. Yanga tukaona ni muhimu kuja na shule ya watoto ya soka,” amesema.

Post a Comment

0 Comments