Yanga Kufungua Yanga Soccer School, Eng Hersi Afunguka Kutumiza Maono yake

Yanga Kufungua Yanga Soccer School, Eng Hersi Afunguka Kutumiza Maono yake

 

Wakati klabu ya Yanga Sc ikitarajiwa kuzindua Yanga Soccer School leo Novemba 15, 2025, Rais wa klabu hiyo, Eng. Hersi Said amesema mpango huo wa kuimarisha muundo wa soka la vijana ulikuwa moja ya vipaumbele vyake vitano alivyovitaja wakati anagombea Urais wa klabu hiyo mnamo mwaka 2022.

Eng. Hersi amesema klabu hiyo imefanya Maendeleo makubwa katika vipaumbele hivyo vikiwemo vingine kama Miundombinu, Mabadiliko, Uthabiti wa Kifedha na Ushirikiano wa Mashabiki huku akitarajia kufikia maono ya muda mrefu kikamilifu kwa kushirikiana na Kamati tendaji ya klabu hiyo.

Eng. Hersi amesema uzinduzi huo itafanyika rasmi leo Novemba 15, 2025 katika Kituo cha SpeedSports Muhimbili Jijini Dar es Salaam ambapo Yanga Soccer School itakuwa katika madaraja ya U-11, U-13, na U-15, ukilenga kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana kwa klabu na taifa.

“Dar es Salaam kama Jiji lenye watu wengi zaidi nchini na Makao yetu Makuu, litatumika kama sehemu ya uzinduzi. Msingi utakapokuwa imara, awamu inayofuata itapanuka hadi mikoani nje ya Dar, kuhakikisha fursa zinawafikia watoto nchi nzima wakiwemo walioko maeneo ya mbali.” amesema Eng. Hersi.

Aidha Eng. Hersi amebainisha kuwa Mgeni Rasmi kwenye hafla hiyo atakuwa Nguli wa soka barani Afrika, kocha Pitso Mosimane ambaye amekuwa rafiki wa muda mrefu kwake na kwa klabu hiyo ambaye uwepo wake kutaongeza thamani ya hafla hiyo kwani ana utaalamu mkubwa kwenye Maendeleo ya soka la vijana.

Mshindi huyo mara tatu wa Ligi ya Mabingwa Afrika, ni mmoja wa makocha wenye mafanikio makubwa zaidi Afrika akishinda Mataji makubwa 21 ndani Afrika na Mashariki ya Kati ana mradi wake wa soka la vijana wa Mosimane Soccer Clinics huko Afrika Kusini aliouanzisha mwaka 2022 na sasa unahudumia zaidi ya wachezaji chipukizi 12,000 na makocha 92.

Post a Comment

0 Comments