
Kocha wa zamani wa Mamelodi Sundowns na Al Ahly ya Misri, Dr. Pitso Mosimane anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa Yanga Soccer School utakaofanyika kesho Novemba 15, 2025 katika kituo maalumu cha kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana cha Speedsports Muhimbili Center.
Mosimane ambaye ni mshindi mara tatu wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) kama kocha ni mmoja wa wataalam wanaoheshimika katika maendeleo ya soka, uwepo wake unatarajiwa kutoa hamasa kwa vijana na wataalamu wa mchezo huo, sambamba na kuonyesha dhamira ya Yanga katika kuwekeza kwenye akademi ya kisasa yenye viwango vya kimataifa.
Mpango huo ambao unalenga vijana chini ya umri wa miaka 11, 13 na chini ya miaka 15 waliopo jijini Dar es Salaam wenye lengo la kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana kwa klabu na taifa, unatajwa kuwa hatua muhimu katika kuhakikisha Tanzania inaendelea kutoa wachezaji bora na kuimarisha misingi ya soka la vijana.
0 Comments