
TIMU ya JKT Queens imetupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake baada ya kuchapwa mabao 4-1 na mabingwa watetezi, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika mchezo wa Kundi B leo Uwanja wa Suez Canal mjini Ismailia nchini Ismailia.
JKT Queens waliuanza vyema mchezo na kufanikiwa kupata bao la kuongoza kupitia kwa kiungo mshambuliaji Stumai Abdallah Athumani dakika ya 12.
Lakini TP Mazembe ikazinduka na kufunga mfululizo kupitia kwa kiungo mzawa, Marlene Yav Kasaj mawili yote kwa penalti dakika ya 23 na 66, mshambuliaji Mnigeria, Samuel Oluwayemis dakika ya 29 na kiungo Mghana, Grace Acheampong dakika ya 45.
Mechi nyingine ya Kundi B leo ASEC Mimosas ya Ivory Coast imeichapa Gaborone United ya Botswana mabao 4-0 Uwanja wa Right to Dream, October Gardens.
Kwa matokeo hayo, ASEC Mimosas inamaliza kileleni mwa Kundi B kwa pointi zake saba, ikifuatiwa na TP Mazembe pointi sita na zote zinafuzu Nusu Fainali, wakati JKT Queens iliyomaliza na pointi mbili nafasi ya tatu na Gaborone United iliyoshika mkia kwa pointi yake moja zote zinaaga michuano hiyo.
Katika Kundi A, AS FAR Rabat ya Morocco imeongoza kwa pointi zake saba ikifuatiwa na wenyeji FC Masar waliomaliza na pointi tano na wote wamefuzu Nusu Fainali dhidi ya USFAS Bamako ya Mali yenye pointi nne na 15 de Agosto Femenino ya Angola ambayo haikuna pointi hata moja.
0 Comments