
Mshambuliaji wa Al-Nassr FC, Cristiano Ronaldo, 40, ameibua mjadala kuhusu kiwango cha umaarufu wake duniani, hatua inayomuibua pia staa wa Bongofleva, Diamond Platnumz, 36, kwa upande wa Tanzania.
Ronaldo, mshindi wa Ballon d'Or mara tano, katika mahojiano ya hivi karibuni na Piers Morgan kupitia kipindi cha Piers Morgan Uncensored, alidai hakuna mtu yeyote duniani ambaye ni maarufu kumzaidi!
Kauli ya CR7 ilikuja wakati wakijadili kitendo cha Rais wa Baraza la Ulaya, Antonio Costa, kumpa Rais wa Marekani, Donald Trump jezi ya timu ya taifa ya Ureno iliyosainiwa na Ronaldo wakati wa mkutano wa G7.
"Ninyi wawili ndio watu maarufu zaidi duniani," Morgan alimwambia Ronaldo, mshindi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA CL) mara tano.
Ili kuipamba hoja yake, Morgan aliongeza kuwa Ronaldo ndiye mtu anayefuatiliwa zaidi katika mtandao wa Instagram akiwa na wafuasi zaidi ya milioni 650, ukilinganisha na Trump mwenye milioni 38
Kisha Ronaldo akauliza, "Tufanye mjadala wa dunia; Ni nani maarufu zaidi, mimi au Donald Trump?" Morgan akajibu kwa utani, "Unadhani ni nani." Ronaldo kwa kujiamini akasema, "Mimi".
"Nadhani duniani kote, hata katika visiwa vidogo, wananijua zaidi yake... Nadhani duniani hakuna mtu maarufu zaidi yangu. Niambie mmoja, niambie mmoja maarufu zaidi!" alieleza Ronaldo.
Akimjibu Ronaldo, Morgan aliwataja watu watatu ambao katika maisha yake anaamini wangekuwa maarufu zaidi kama wangekuwa hai hadi sasa. Watu hao ni Princess Diana, Malkia Elizabeth II, na Nelson Mandela.
Kisha akaongeza, "Lakini kwa sasa, ni wewe na Donald Trump." Ronaldo akajibu, "Ni mjadala mzuri.".
Nami naendeleza mjadala huo mzuri. Mbali na mafanikio katika soka, Ronaldo anaamini kuwa na wafuasi wengi katika mitandao duniani, ni sehemu ya uthibitisho kuwa yeye ndiye mtu maarufu zaidi ulimwenguni.
Ikumbukwe Ronaldo ni namba mmoja duniani kwa wafuasi wengi Instagram (milioni 667), Facebook (milioni 171), huku akishika namba tatu X, zamani Twitter (milioni 112), na nafasi ya 32 YouTube (milioni 77.1).
Kwa Tanzania, Diamond, mwanzilishi wa WCB Wasafi, ndiye anayeongoza katika mitandao ya kijamii. Je, kwa kutumia kipimo cha Ronaldo na Morgan tunaweza kusema mwanamuziki huyo ndiye mtu maarufu zaidi nchini?.
Diamond, mshindi wa Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) mara 22, tangu alipotoka na wimbo wake, Kamwambie (2009) na kushinda tuzo ya kwanza kama Msanii Bora Chipukizi, jina lake limeendelea kuwa juu kimuziki.
Wiki mbili zilizopita akifunga kampeni za Uchaguzi Mkuu mkoani Kigoma ambapo alienda kumuunga mkono Baba Levo, Diamond alijitaja kama mwanamuziki namba moja Tanzania!.
"Leo katika nchini hii mimi ndiye mwakilishi wa kwanza katika muziki... Kama kuna kiumbe chochote nchi hii kinafanya muziki kinaniweza kisogee mbele yangu," alisema Diamond.
Kwa kutazama namba za wasikilizaji (streaming) wa nyimbo zake katika majukwaa yote ya kidijitali, hakuna ubishi kuwa Diamond ndiye namba moja kwa wakati huu.
Mathalani ndiye mwanamuziki namba mbili kwa kutazamwa zaidi YouTube ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, akiwa ametanguliwa na mshindi wa Grammy kutokea Nigeria, Burna Boy.
Pia Diamond anaongoza kwa kushinda tuzo nyingi za TMA kwa muda wote, na za kimataifa, miongoni mwa hizo ni Channel O, Trace, Soundcity, Headies, AFRIMMA, Kora, AEAUSA, the HiPipo Music na AFRIMA.
Kubwa zaidi ni kushinda tuzo tatu za MTV EMAS (MTV Europe Music Awards) - akiwa amelingana na mshindi wa Grammy kutokea Afrika Kusini, Tyla.
Anasifika kwa kufungua miradi ya kibiashara nje ya muziki, mathalani ndiye msanii wa kwanza Tanzania kumiliki vyombo vya habari, ambapo anatajwa kuwa wa pili Afrika baada ya Youssou N'Dour wa Senegal.
Mafanikio ya muziki wake yamemfanya Diamond kujizolea mamilioni ya wafuasi katika mitandao ambapo amekuwa namba moja nchini kwa takribani mitandao yote ya kijamii.
Diamond ni namba moja Instagram (wafuasi milioni 18.7), Facebook (milioni 7.5) na YouTube (milioni 10.7), huku akishika namba nane X, zamani Twitter (milioni 1.3), na namba mbili TikTok (milioni 10).
Ikiwa Ronaldo anaamini yeye ndiye mtu maarufu zaidi duniani akitumia ushawishi wake katika mitandao kama moja wapo ya njia ya kuthibitisha hilo, vipi kuhusu Diamod kwa hapa Tanzania?.
Kumbuka watu wengi sasa wanatumia mitandao - kulingana na takwimu za hivi karibuni kutoka Kepios, zinaonyesha hadi kufikia Oktoba 2025, watumiaji wa mitandao ya kijamii duniani kote walifikia bilioni 5.66.
Watu hao hutumia wastani wa saa 18 na dakika 36 kwa wiki wakiwa kwenye mitandao wakitazama picha na video kwenye majukwaa ya YouTube, TikTok, Instagram na Facebook.
Kwa ujumla, dunia nzima hutumia takribani saa bilioni 15 kila siku ikitazama na kutuma maudhui kwenye mitandao ya kijamii, ikiwa sawa na zaidi ya miaka milioni 1.7 ya uwepo wa binadamu!.
Vilevile asilimia 93.8 ya watumiaji wa intaneti duniani, bila kujali umri, hutumia mitandao ya kijamii kila mwezi, huku idadi ya watu wazima (kuanzia miaka 18) wanaotumia mitandao ikifikia asilimia 92.6 ya watu wote katika kundi hilo.
0 Comments